Baraza la Kitaifa la kutafsiri sheria za Kiislamu nchini Kenya (Kenya National Fatwa Council) limetoa wito kwa serikali kutangaza Alhamisi ijayo kuwa sikukuu ya kuadhimisha Eid ul Adh-ha.
Naibu Mkurugenzi wa baraza hilo Sheikh Abubakar Bini anasema tayari Waislamu nchini wameanza kuadhimisha siku kumi za mwezi mtukufu wa 12, na kuwa hii leo, Jumatano, ni siku ya pili.
Bini akizungumza mjini Eldoret amesema kuwa kama baraza, wamekubaliana kuwa sherehe za Eid ul Adh-ha mwaka huu zitakuwa Alhamisi kwa mujibu ya mwandamo wa mwezi katika eneo la Afrika Mashariki.
“Ombi letu kwa serikali ya Rais William Ruto ni kuwa Idd iwe ni sikukuu na iwekwe tarehe 29. Hii itaafikiana na sherehe za Africa Mashariki kwa kuwa Tanzania na Zanzibar wanasherekea siku hiyo,” alisema Naibu Mkurugenzi huyo wa baraza la Fatwa.

Eid ul Adh-ha ni mojawapo ya sherehe muhimi za dini ya Kiislamu.
Wakati wa sherehe hizo, Waislamu ambao hawakupata nafasi ya kuenda Hiji hutakiwa kutekeleza ibada mabali mbali ikiwemo ile ya kuchinja na kusoma Kurani.
“Haji inakua tarehe kumi ya mwezi wa kwanza kulingana na kalenda ya Kislamu na wale ambao hawajabahatikiwa kuende kutekeleza nguzo hiyo inawapaswa wafanye bidii kutekeleza ibada mbali mbali kama vile kusaidia wasiojiweza, kufunga saumu na kusoma kurani,” Sheikh Bini alieleza.
“Ni siku kumi muhimu. Siku zinaanza kulingana na muandamo wa mwezi,” aliongezea.
Hali ngumu ya kiuchumi
Kwa kuchinja, Waislamu hufuata mwendo wa Mtume Ibrahimu ambaye alijitolea kumchinja mwanawe Ismaeli lakini Mungu akaleta kondoo kutoka mbinguni.

kutokana na hali ngumu ya kiuchumi, Bini anakiri huenda sherehe hizo zikaathirika.
Hata hivyo, ametoa wito kwa waislamu wenye uwezo kuhakikisha wanashiriki katika sherehe hizo kwa kuchinja ili kuwasaidia wasiojiweza katika jamii.
“Uchumi ulivyo sasa, tunaomba wale ambao wamebahatikiwa na mifugo watoe katika kuchinga ili kusaida wale hawana. Haimmaanishi uchumi ni migumu kwa hivyo tusisherekee,” alisema Naibi Mkurugenzi wa Baraza la Fatwa.
Baraza hilo sasa lina imami Waziri wa Mambo ya Ndani Prof Kithure Kindiki ataskiza ombilao na kutangaza tarehe 29 mwezi Juni kuwa siku ya sherehe za Eid ul Adh-ha.
Kisheria, waziri Kindiki ndiye mwenye mamlaka ya kutangaza sikukuu ya kitaifa.


