Baraza la kitaifa la Fatwa limepongeza Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) kwa kuendesha zoezi la uwazi la kumteua Kadhi Mkuu mpya nchini.
Naibu Mkurugenzi wa Baraza hilo Sheikh Abubakar Bini aidha amesema wamekaribisha uteuzi wa Athman Abdulhalim Hussein kwa wadhfa huo.
JSC ilitangaza uteuzi wa Hussein Jumatatu baada ya kukamilika kwa mahojiano ya waliotuma maombi.
“Sisi kama Kenya National Fatwa Council tunapongeza JSC Kwa kufanya uteuzi kwa uwazi. Huyu ambaye ameteuliwa ameshinda kwa sababu ya ujuzi na uadilifu wake,” Bini aliambia Uasin Gishu News.

Halkadhalika, amesema mwenyekiti wa Fatwa Ahmad Sharif Ahmad pia ameunga mkono uteuzi wake.
Hussein anachukua nafasi ya Ahmed Muhdhar ambaye MDA wake wa kuhudumu ulikamilika mwezi Disemba mwaka Jana.
“Tuko tayari kufanya kazi na Kadhi Mkuu mpya ili kuwaleta waislamu pamoja,” ameongeza.
Baraza hilo ambalo linatoa ushauri kwa maswala ya Kiislamu nchini sasa linamtaka Hussein kufuata nyayo za Kadhi Wakuu waliomtangulia.
Kadhi Mkuu wa kwanza nchini Kenya aliteuliwa mwaka 1963.
Mahakama ya Kadhi
Hata hivyo, Baraza La Fatwa linataka kitengo cha rufaa katika mahakama ya Kadhi nchini kubuniwe.

Kwa sasa kuna Mahakama ya Kadhi ambapo uamuzi wake unaeza kupingwa katika mahakama Kuu ya kawaida.
“Kadhi Mkuu ni cheo kikubwa lakini cha kushangaza ni kubwa hatuna mahali pa kukata rufaa kwa waislamu. Kama mtu hajaridhika na uamuzi wa Mahakama ya Kadhi hana pa kuenda,” alisema Sheikh Bini.
“Tunaiomba serikali kupitia kwa Jaji Mkuu Martha Koome, aliangalie swala hili la kutupatia Mahakama ya Appeal ili dini yetu ipate kuendelea kwa njia ambayo inastahili,” aliongeza.


